Ayatullah Ahmad Jannati, Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kifo cha Kanali Muammar Gaddafi dikteta wa zamani wa Libya kimeleta furaha kwa watu wote wanaodhulumiwa ulimwenguni. Ayatullah Jannati ameashiria tuhuma za hivi karibuni za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kubainisha kwamba, kazi ya Marekani daima ni kutoa tuhuma na siku zote imekuwa ikitumia wenzo huu. Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya Marekani kutumia wenzo wa propaganda na tuhuma dhidi ya Iran lakini siku zote imekuwa ikishindwa na taifa hili. Ayatullah Ahmad Jannati ameashiria pia matukio ya hivi sasa katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kukosoa siasa za kindumakuwili za Wamagharibi kuhusiana na matukio haya.